emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

WAKALA WA HUDUMA YA UNUNUZI SERIKALINI

Ununuzi Unaozingatia Thamani

Habari

    WAZIRI WA FEDHA MH DKT MWIGULU NCHEMBA ASISITIZA MAONO YA MH. RAIS DKT SAMIA SULUHU HASSAN MIFUMO ISOMANE KATIKA UTENDAJI KAZI WA SERIKALI (UZINDUZI MFUMO WA GIMIS).

  • 24-Oct-2023

Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. @mwigulunchemba (Mb) ameielekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma @ppra_tanzania kuhakikisha inaunganisha mfumo mpya wa kielektroniki wa Ununuzi wa Umma wa NeST na mfumo wa utoaji huduma za Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini wa GIMIS ili kurahisisha mchakato wa Ununuzi Serikalini.

Waziri Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb) alitoa maelekezo hayo wakati akizindua mfumo jumuishi wa kielektroniki wa utoaji huduma za Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini ujulikanao kama GIMIS (GPSA Integrated Management Information System) uliofanyika siku ya Jumamosi tarehe 21/10/2023 katika ukumbi wa Kambarage-Hazina jijini Dodoma.

Alisema PPRA iunganishe mifumo hiyo haraka iwezekanavyo kwa kuwa mfumo wa GIMIS unatumiwa na Wizara, Mashirika ya Umma, Wakala za Serikali, Ofisi za Mikoa na Halmashauri za Wilaya Nchini katika kupata huduma za GPSA.

"Mheshimiwa Rais Dkt. @samia_suluhu_hassan amekuwa akisisitiza mifumo ya Serikali isomane hivyo ni muhimu mifumo mingine ihakikishe inaunganishwa na GIMIS ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini", alibainisha Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba.

Alisema kuwa mfumo wa GIMIS utaongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Wakala kwa kuwa majukumu yote ya Wakala yanatekelezwa ndani ya mfumo huo.

Aidha, Dkt. Nchemba alitoa wito kwa Taasisi Nunuzi kuhakikisha wanatumia huduma za GPSA kwa kuwa Sheria ya Ununuzi na Kanuni zake inazitaka kupata huduma na Vifaa Mtambuka kupitia GPSA.

Aliipongeza GPSA kwa kukamilisha ujenzi wa mfumo huo na majengo ya Ofisi na vituo vipya vya mafuta vya Songwe, Simiyu, Pwani na Dodoma pamoja na kufanya ukarabati katika Ofisi za Mikoa 17 na kusimika matenki ya mafuta katika Mikoa 12, kwa kuwa hatua hiyo itaongeza mapato na morali ya utendaji kazi kwa watumishi.

Mheshimiwa Dkt. Nchemba pia aliipongeza GPSA kwa kuendelea kuchangia katika Mfuko Mkuu wa Serikali ambapo katika kipindi cha miaka mitano mpaka kufikia mwaka 2022/23 imechangia kiasi cha shilingi Bilioni 11.9.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mheshimiwa George Simbachawene alisema mfumo huo umeshaunganishwa na Mfumo Mkuu wa Serikali ambao unaiwezesha mifumo kubadilishana taarifa na umeshaanza kubadilishana na baadhi ya mifumo ya Taasisi za Umma ikiwemo Mfumo wa Kukusanya Mapato ya Serikali (GePG) na mfumo wa Usimamizi wa Rasilimali za Serikali.

Aliongeza kuwa jitihada zinaendelea kuunganisha mfumo huo na mifumo mingine ya Serikali kulingana na mahitaji ya ubadilishaji wa taarifa na kubainisha kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya Kisera na Kisheria kuwezesha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kusimamia masuala ya Serikali Mtandao kwa ufanisi.